Mageto’ Kishapu yachochea mimba za wanafunzi shuleni
CHANGAMOTO ya uhaba wa mabweni kwenye shule nyingi za sekodari za Kata, bado ni janga linalowaathiri zaidi wanafunzi wa kike.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bunambiyu wilayani Kishapu, akiwa amebeba Bango likionyesha namna umbali mrefu kwenda shule ulivyo kikwazo kwa wanafunzi
Kimsingi uwepo wa mabweni katika shule hizo ni suluhisho tosha dhidi ya madhira yanayowakabili wanafunzi wa kike ambao baadhi hukaa mbali na shule, hali inayosababisha waingie katika mitego mbalimbali ikiwamo ya kutongozwa, kubakwa na mbaya zaidi kupata ujauzito.
Serikali ilianzisha shule hizo kwa lengo la kuongeza wigo wa wanafunzi wanaoingia elimu ya sekondari, baada ya shule ya msingi ili kukuza kiwango cha elimu nchini.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alisema Agosti 25, 2014, kwamba wakati anaingia madarakani 2005, ni asilimia 10 tu ya wanafunzi walikuwa wakichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari kwenye shule za Serikali, kutokana na uchache wa shule hizo.
“Kwa miaka mingi hatukujenga shule mpya za sekondari na kama mnavyojua wakoloni wa Kiingereza, ndio kabisa hawakujenga shule… kazi hiyo waliwaachia Wamisionari,” anasema na kuongeza:
“Kwa hiyo wakati tunaingia madarakani, hali ilikuwa mbaya… ndio maana tukaja na sera ya kujenga shule za Kata,” anasema.
Aidha, Sera hiyo kwa asilimia kubwa imefanikiwa baada ya kujengwa kwa shule nyingi za Kata ambazo zimetoa fursa ya elimu ya sekondari kwa wanafunzi wengi, katika dhima nzima ya kupambana na adui ujinga.
MAGETO
Sasa kutokana na changamoto ya uhaba wa mabweni na hasa kwa wanafunzi wanaotoka mbali na shule, wakati mwingine kwa umbali wa hadi kilometa 15 kwenda na zingine 15 kurudi nyumbani, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakilazimika kupanga vyumba vya kuishi uraiani, maarufu kama ‘Mageto’ ili kuwa karibu na shule.
Tofauti na matarajio ya wengi, wazazi wakiwamo kwamba kupanga vyumba karibu na shule na hasa kwa wanafunzi wa kike kunaboresha taaluma yao, wengi wamejikuta wakipewa ujauzito na hivyo kukatishwa masomo yao.
Aidha, wengine wameishia kuwa vimada wa wanaume, wakisoma shule huku wameolewa.
Miongoni mwa shule zinazokabiliwa na kadhia hii ni shule ya Sekondari ya Kata Bunambiyu, iliyo katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Hii ni miongoni mwa shule za Serikali zisizo na mabweni, huku baadhi ya wanafunzi wake wakiwa wamepanga Mageto uraiani.
Inaripotiwa kuwa kwa mwaka huu wa 2018, tayari wanafunzi watano katika shule hiyo waliopanga uraini (Mageto) wameshapewa ujauzito na kukatishwa masomo yao.
Na hiyo inatokana na wanafunzi hao kuishi kwa kujitawala bila ya uangalizi wa wazazi ama walimu.
MWALIMU
Fransic Mtambo ni mwalimu katika shule hiyo. Anasema awali kulikuwa na bweni lakini liliungua moto mwaka jana, hali iliyolazimu baadhi ya wanafunzi wanaotoka mbali, wapange vyumba uraiani ili kuwa karibu na shule.
Anasema kabla ya bweni hilo kuungua, shule haikuwa na tatizo la wanafunzi kupewa ujauzito, lakini baada ya kukosekana kwa bweni na wanafunzi kupanga vyumba uraiani, tayari matatizo yameshaanza kutokea na kwamba hadi sasa wanafunzi watano wameshapewa mimba na kuacha masomo.
“Mwanafunzi anapopanga uraiani (Geto), anakuwa huru zaidi tofauti na anapokuwa akiishi na wazazi wake ama chini ya uangalizi wa walimu,” anasema na kuongeza:
“Anakuwa akijitawala na kuamua kufanya jambo lolote bila ya kujua madhara yake ya baadaye, na ndiyo maana idadi kubwa ya wanafunzi waliopanga uraiani wanaambulia ujauzito.”
WITO
Mwalimu Mtambo anatoa wito kwa serikali na wadau wa elimu kwa ujumla kutoa msukumo wa ujenzi wa mabweni kwenye shule za kata kama ilivyofanya kwenye utengenezaji wa madawati.
“Likifanyika hili, litanusuru wimbi la wanafunzi kukatishwa masomo sababu ya kupewa ujauzito,” anasema.
MWANAFUNZI
Amina Kisena ni miongoni mwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Bunambiyu, waliopanga vyumba uraiani akiwa kidato cha nne.
Anasema kuwa kupanga chumba uraiani ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi wa kike na hasa ya kuambulia ujauzito na kukatishiwa masomo yao.
Anabainisha kwamba mwanafunzi wa kike anapokuwa amepanga chumba ni rahisi kurubunika na hasa pale anapokuwa ameishiwa pesa ya matumizi.
“Ni rahisi kwake kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi ili tu aweze kutatua changamoto inayomkabili, na mwisho wa siku anajikuta tayari ameshapewa ujauzito,” anasema na kuongeza:
“Kwa kweli tuliopanga kwenye Mageto, tupo huru sana na wanaume wanachukulia hiyo kama fursa ya kutupata kirahisi, na hasa mtu anapokuwa hana hela za matumizi na wazazi wamechelewa kumtumia, anajikuta anamkubali mwanaume ili tu asilale njaa.”
Amina anabainisha kuwa kuna wanafunzi wenzao wanaoishi kimada na wanaume wakiwa bado wanasoma.
“Anatoka shule, anarudi kwa mumewe huku wazazi wakiwa hawajui, sababu wengi wao hawana tabia ya kutembelea watoto ili kuona namna wanavyoishi pamoja na kufuatilia maendeleo yao shuleni…wao ni kutuma pesa tu basi,” anasema.
Anakiri kwamba maisha ya Geto si mazuri kwa wanafunzi, ambapo licha ya kuambulia ujauzito, kitaaluma pia wamekuwa wakishuka kwa kufanya vibaya kwenye masomo yao, sababu ya kukosa usimamizi wa kujisomea masomo.
MZAZI
Mmoja wa wazazi Rebeka Kisena anawataka wazazi wenzake ambao watoto wao wamepanga vyumba uraiani waache tabia ya kuwatelekeza.
“Wawe wanawatembelea siku za mwishoni mwa juma ili kujua maisha wanayoishi pamoja na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi, na madhara ya kufanya mapenzi wakiwa wanafunzi,” anasema.
MWENYEKITI
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bunambiyu eneo ambalo wanafunzi wengi wamepanga uraiani Elisha Simoni, anakiri baadhi ya wanafunzi kuwa vimada wa wanaume.
Anabainisha kuwa tayari walishafanya mikutano ya hadhara na wananchi na kuonya juu ya tabia ya kutongoza wanafunzi.
Simoni anasema serikali ya kijiji inajitahidi kudhibiti vitendo hivyo, lakini inaonekana kugonga mwamba kwa sababu ya wanafunzi wanakubaliana na hali ya kufanya mapenzi na wanaume.
“Wanakubali vitendo hivyo wakati mwingine ili wapate pesa pamoja na kununuliwa simu za mkononi hasa Smartphone, na hivyo kujikuta wakiambulia ujauzito,” anasema.
DIWANI
Richard Sangisangi ni Diwani wa Kata hiyo ya Bunambiyu.
Anasema kutokana na vitendo vya wanafunzi kupewa mimba, tayari baadhi ya wananume wameshakamatwa na kupelekwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wanaolaghai wanafunzi.
“Ukosefu wa bweni katika shule yetu hii ya Sekondari Bunambiyu ndio umechangia mambo yote ya wanafunzi kupewa ujauzito, sababu ya kuishi kwenye mageto,” anasema na kuongeza:
“Hatua ambayo tumeichukua ni kuhakikisha tunajenga bweni jingine na kwamba fedha ya kazi hiyo kwenye halmashauri yetu ipo,”anasema.
OFISA MAENDELEO
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Joseph Swalala, anakiri uwapo wa changamoto hiyo ya mabweni kwenye shule za kata unachangia kukithiri kwa mimba shuleni, na hatimaye wanafunzi kukatishwa masomo yao.
Anasema mpango uliopo ni kuhamasisha wananchi washirikiane na serikali kuhakikisha shule zote za kata wilayani humo zinajengewa mabweni, ili kunusuru mimba shuleni.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Save the Children mkoani Shinyanga, Benet Malima, ambao wanatekeleza Mradi wa Kupinga Mila na Desturi Kandamizi kwa watoto wa kike katika Kata hiyo ya Bunambiyu, anawaasa wanaume kuacha tabia ya kutongoza wanafunzi.
“Ni muhimu wawaone kama watoto wao wa kuwazaa ili wapate kutimiza ndoto zao na taifa lipate kuwa na wasomi wa jinsia zote mbili, wa kiume na wa kike,” anasema.
Comments
Post a Comment