NILIKUPENDA ZAIDI WEWE.
NILIKUPENDA ZAIDI WEWE.
Hapo kale, alikuwapo msichana mrembo - kipofu. Kwa sababu ya upofu wake, alijichukia sana na kujikatia tamaa. Chembe pekee ya furaha aliyobakiwa nayo moyoni, ilitokana na upendo wa hali ya juu aliokuwa akitendewa na mpenzi wake. Alipendwa, alithaminiwa, alidekezwa na kuengwaengwa mithili ya mboni ya jicho. Ikafikia hatua, kwa mapenzi aliyopewa, msichana akaweka nadhiri kwamba, siku akibahatika kufumbua macho na kuiona dunia, basi ataolewa na mpenzi wake huyo bila mahari.
Siku moja, alitokea mtu ambaye - inasemekana - alikuwa katika saa za mwisho wa uhai wake, akaamua kujitolea macho yake akampa msichana huyu, kwakuwa yeye hakuwa na maisha marefu tena. Na baada ya madaktari kumfanyia upasuaji msichana, na kumpandikizia macho yale, hatimaye msichana alifanikiwa kuona; aliona kila kitu pamoja na kumwona mpenzi wake.
Mpenzi wake akamuuliza, "Hatimaye umeiona dunia. Je, uko tayari sasa kufunga ndoa nami?"
Msichana alifadhaika mno baada ya kugundua kwamba, kumbe mpenzi wake naye alikuwa kipofu. Hakuvutiwa naye, hakuwa tayari kumhudumia mtu asiyeona. Msichana akagoma - si tu kuolewa bila mahari - bali kuolewa kabisa na kijana yule. Kwa simanzi na fadhaa, kijana aliondoka huku akilia kwa uchungu.
Baada ya kupita mwezi mmoja, kijana alifariki kwa kihoro. Wakati wa mazishi, ikawa bahati, yule msichana akahudhiria msibani. Alipofika tu, wafiwa wakamkabidhi barua aliyoachiwa na marehemu. Katika barua hiyo, marehemu alisema:
"Mpenzi, tafadhali yatumie vizuri macho yangu, sikuyatoa na kukupa kwa sababu siyapendi au siyahitaji, bali ni kwa sababu nilikupenda zaidi wewe!"
Msichana aliishiwa nguvu na kuanguka chini papo hapo!
Comments
Post a Comment